Joseph Mbilinyi, mmoja wa wabunge vijana wapya kutoka kambi ya upinzani BAADHI ya wabunge vijana wa vyama vya upinzani wamelaani kauli iliyotolewa na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashililah na kueleza kuwa wao ni vinara wa sheria na kanuni kuliko hata Spika wa Bunge, Bi. Anna Makinda.
Vile vile wameahidi katika bunge la bajeti watatoa hoja bungeni na kumtaka katibu huyo kufuta na kuomba radhi kwa kauli yake ya kuwaita wabunge mbumbumbu wa sheria na kanuni.
Dkt. Kashililah akizungumza na vyombo vya habari juzi, alisema kuwa vitendo vya fujo na kutoleana maneno ya kejeli baina ya wabunge wakiwamo ndani ya bunge, ni matokeo ya kuwepo kwa wabunge wengi wapya na wasiojua vema sheria na kanuni za bunge.
Wabunge hao walisema kuwa kauli ya Katibu wa Bunge imewadhalilisha wao, bunge na wananchi kwani amedharau wananchi kwa kuwa wamechagua wawakilishi mbumbumbu wa sheria na kanuni.
Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA), Bw. Ezekia Wenje alisema kuwa katika bunge la mwezi wa sita atapeleka hoja bungeni ya kumtaka Katibu huyo wa Bunge kuomba radhi na kufuta kauli yake hiyo.
"Kutuambia wabunge ni mbumbumbu ni madharau makubwa sana na utovu wa nidhamu. Zile kanuni si dictionary wala biblia, huhitaji mwezi mzima kujifunza, ni ndani ya wiki moja tu umeshajifunza kwani ni kajitabu kadogo sana," alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Wenje, wabunge vijana hawakubali kuburuzwa bungeni na wanakuja juu pale wanapoona kanuni zinavunjwa kwa manufaa ya kundi fulani.
"Wakiona wamebanwa kwenye vifungu, wanaamua tu kutengua kanuni, sisi hatutakubali na hatutanyamazishwa, tutaendelea kusema," alisema.
Mbunge wa Mihambwe (NCCR-Mageuzi), Bw. Felex Mkosamali alisema kuwa kwa upande wake amesoma sheria na kanuni na kufauli vizuri masomo hayo, hivyo anao uwezo mkubwa na upeo wa masomo hayo.
"Mtu kama mimi ni mwanasheria nimeenda darasani na maprofesa wamenipa A kwenye masomo hayo, sasa anataka hawa maprofesa kutuambia hawana akili?
"Spika tunajua si mwanasheria na ndiyo maana mbunge anapotoa hoja anamkatisha kabla hajamaliza. Tunaijua sheria na kanuni kuliko huyo spika anayemtetea," alisema Bw. Mkosamali wakati akizungumza na gazeti hili jana.
Aliongeza kuwa kauli ya Bw. Kashillilah imewadhalilisha na kusisitiza kuwa, kwa kuwa kipimo cha kwenda shule ni vyeti, hivyo alimtaka Spika kutoa vyeti vyake alivyosomea masomo hayo ili vilinganishwe na vya kwake.
"Wametudhalilisha sana, nia yao wanataka kutunyamazisha tukiwa bungeni...mwezi wa sita tunakwenda kuwasha moto ndani ya bunge," alisema.
Mbunge mwingine wa NCCR-Mageuzi wa jimbo la Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila, hali kadhalika alilaani kauli hiyo na kusema kuwa fujo ndani ya bunge hazisababishwi na wabunge vijana tu, kwani wapo wazee wa siku nyingi ambao wamekuwa vinara wa fujo ikiwa ni pamoja na kutojua kanuni na sheria.
Alisema alichotakiwa kusema Katibu wa Bunge ni kuwataja wale wasiojua kanuni na sheria lakini anaposema wabunge wapya hawazijui, ni kuwadhalilisha wao na bunge lenyewe.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Bi. Ester Bulaya naye alipinga kauli ya Katibu huyo wa Bunge kuwa tatizo si kutozijua kanuni, bali wengi wa wabunge wanashindwa kutawala jazba zao na baadhi wana uchanga wa kisiasa.
Hata hivyo alisisitiza umuhimu wa wabunge kuendelea kujifunza taratibu za bunge ili waweze kutoa hoja za msingi huku wakizuia jazba zao. |
No comments:
Post a Comment