Monday, April 25, 2011

Neno La Leo: Utajuaje Mtu Mwongo Anaposema Ukweli?


Ndugu Zangu,

TUMETOKA kusheherekea Pasaka. Na Pasaka ni wakati pia wa kutafakari. Ndio, ni wakati wa kufikiri. Na si kufikiri tu, bali kufikiri kwa bidii.

Maana, Bwana Yesu alifanyiwa matendo maovu na watu aliowaamini. Yuda ni mmoja wa watu hao. Si tunafahamu, kuwa Yuda naye alimsaliti Bwana Yesu. Kwanini Yuda alimsaliti Yesu? Tafakari.

Pasaka imetukumbusha na itaendelea kutukumbusha, kuwa katika dunia hii, miongoni mwetu kuna watu waongo. Ni watu walaghai, wenye ghilba nyingi. Ni watu wenye kuwadhulumu wenzao. Marehemu Remmy Ongala alipata kuimba; “ Kuna wengine watu hudhulumu wenzio wao, kwa uongo wao, kwa vyeo vyao kazini, kwa rushwa zao, kwa ujanja wao….!

Ndio, Remmy Ongala aliizungumzia jamii aliyoiona wakati huo. Na labda leo Remmy angeimba; “ Kuna wanasiasa wenye kudhulumu watu wao, kwa ubinafsi wao, kwa tamaa zao, kwa ufisadi wao, kwa uroho wao wa madaraka…!”

Na swali ni hili; Utajuaje kuwa mtu mwongo amesema ukweli?
Jibu: Utambue, kwa wengine uongo ni tabia- habitual. Mtu mwongo kwa tabia siku zote atasema uongo. Mathalan, hata anapokutana na mwanamke au mwanamme, kwanza anafikiri namna atakavyomdanganya. Hata kama ni mapenzi, atafikiri namna ya kumdanganya kimapenzi. Na kama ni mwanasiasa vivyo hivyo, anapokutana na wananchi, kichwani atafikiria na kujiuliza; watu hawa nitawadanganya na nini?

Na mtu mwongo kwa tabia anaposema uongo na kisha kukiri mbele yako huku akikutazama machoni kwa kukwambia; “ Sahamani, nimeongopa”. Basi, hapo uamini, kuwa mtu mwongo kwa tabia atakuwa amesema ukweli katika sentesi hiyo tu, kuwa; “ Samahani, nimeongopa”.

Baada ya sentesi hiyo usije ukadhani, kuwa yatakayotoka kinywani kwake yatakuwa ni ya ukweli! Na hili ni Neno La Leo.

Maggid
Iringa,
Jumanne, Aprili 26, 2011

No comments:

Post a Comment